Ni kwa jinsi gani msomi anavyoweza kuleta mabadiliko chanya na pia
kuleta hasara au kuwa chanzo cha matatizo ndani ya Jamii.
Msomi ni mtu mwenye elimu ya jambo fulani. Katika nchi za
kiafrika, kiwango cha elimu kimekuwa si cha kuridhisha ukilinganisha na nchi zilizoendelea. Hali hii imezifanya serikali
za nchi mbalimbali za kiafrika kutilia mkazo katika suala la elimu kwani elimu
ni kiungo muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo katika nchi yoyote duniani. Uchambuzi wa
mada hii, unaegemea zaidi katika nchi zinazoendelea hasa za kiafrika na Tanzania
ikiwemo.
Msomi anafaida kubwa na nafasi ya kuleta mabadiliko chanya ndani
ya jamii. Umuhimu wa msomi ndani ya jamii ni pamoja na kufanya kazi mbalimbali
za kitaalamu kama vile; udaktari, ualimu, uhandisi nk. Ufanyaji wa kazi hizi
unapelekea kupata maendeleo na pia jamii kwenda sambamba na mabadiliko ya
sayansi na technolojia.
Umuhimu mwingine wa msomi ni pamoja na kuwa mshauri ndani
ya jamii katika mambo mbalimbali kama vile; kuwasadia wasio na elimu kwa kuwaelekeza
njia bora za kufuata katika jambo fulani. Kwa mfano, msomi mwenye ujuzi na mambo
ya kilimo, anaweza kuwashauri wakulima wanaomzunguka kufuata njia bora za
kilimo kama vile kilimo cha kisasa. Kwa kufanya hivyo, msomi huyo, atakuwa anafaida
kubwa katika jamii inayomzunguka.
Msomi pia anafaida kwani atakuwa ni motisha kwa jamii
inayomzunguka. Hii ina maana kwamba, matendo mazuri atakayokuwa anayafanya
msomi huyu, yatawapa motisha watu wengine ndani ya jamii kwa kuyaiga hivyo
kuleta maendeleo ndani ya jamii husika. Kwa mfano, katika jamii za kijijini
ambako kiwango cha elimu kipo chini, akitokea msomi ambaye amefanikiwa kutokana
na elimu, basi inaweza kuwapa motisha watu wengine kuwapeleka shuleni watoto
wao au wanafunzi wa eneo hilo kusoma kwa bidii ili kuwa kama yeye ambaye
amefanikiwa kutokana na elimu.
Tukiachilia mbali faida za msomi, katika nchi za kiafrika
zinazoendelea hasa Tanzania, msomi anaweza kuwa hatari na chanzo cha matatizo
makubwa ndani ya jamii. Hii ina maana kwamba, msomi asiyemwaminifu anaweza
kutumia elimu aliyonayo kuwadhulum na kuwaibia wanachi wasio na elimu badala ya
kuwasaidia. Hali hii imefikia wasomi kuitwa “majambazi
wa kalamu” Kwa mfano, hapa kwetu Tanzania, mtu akiwa anasoma anakwambia
kabisa, akiajiriwa anachukua chake mapema na akiishaajiriwa anachukua chake
mapema kwa kuiba au kuomba rushwa. Hali hii imepelekea wasomi wasiowaaminifu
kuwa hatari na kukwamisha maendeleo ya
nchi.
Pia, baadhi ya wasomi wamekuwa chanzo cha matatizo ndani ya
jamii ambapo wamekuwa wakitumia elimu yao kwa kuwarubuni au kuwadanganya watu
wasio na elimu. Kwa mfano, msomi anaweza kuwashawishi wanajamii kutoshiriki
jambo fulani lenye manufaa kama vile ujenzi wa shule na wanajamii nao
watamsikiliza kutokana na imani ambayo bado imo miongoni mwa wanajamii wengi kwamba
kile anachokisema msomi ni sahihi.
Matendo maovu ya msomi nayo yanaweza kuwakatisha tamaa wanajamii
kwa kuona kuwa hakuna umuhimu wala maana ya kusoma endapo mtu anasoma halafu
anafanya mambo yasiyo na tija katika jamii. Kwa mfano, unakuta msomi, anakunywa
pombe halafu analala mtaroni, au unakuta msomi anatukana matusi ovyo barabarani
au anaongea vitu visivyo na mantiki. Hali hii hupelekea wanajamii kuona kuwa
hakuna tofauti kati ya aliyesoma na asiyesoma.
Hizi ni baadhi tu ya hasara na faida za msomi katika jamii. Hivyo basi,
wewe kama msomi, unatakiwa uwe mfano mzuri wa kuigwa ndani ya jamii. Kumbuka
kwamba, katika jamii yetu ambayo kiwango cha watu wenye elimu ni kidogo, bado
msomi ana nguvu kubwa ya kuleta mabadiliko chanya au kuiharibu jamii.